Bwana Yesu asifiwe milele!

Tunaamini unaendelea vyema kwa msaada wa uzima wa Yesu Kristo uliomo ndani yako.

Sisi pamoja na timu nzima ya MANA – tunaendelea vizuri na kazi ya kumtumikia Mungu.    Tunamshukuru Mungu kwa kila mtu ambaye anapata nafasi ya kutuombea.

Pamoja na ratiba mbalimbali za kazi za Mungu tulinazo mwezi huu, tutakuwa pia na safari ya kwenda Israeli. Safari hii ya Israeli itakuwa tarehe 6 – 15 juni 2015.

Ndani ya barua hii tunataka tukukumbushe tu umuhimu wa wewe kuzifahamu habari za nchi ya Israeli, na zinavyoweza kukusaidia upate kumjua Mungu zaidi.

Hii ni kwa sababu Mungu alichagua wana wa Israeli kama jamii na Taifa ambalo ameamua kulitumia KUJIJULISHA KWA ULIMWENGU.

Ukiisoma Biblia utaona wazi ya kuwa sehemu kubwa ya vitabu vilivyomo ndani yake vinaelezea juu ya wana wa Israeli na nchi yao ya Israeli.

Mungu anataka ajulikane na watu wake aliowaumba waliomo ulimwenguni.Na njia mojawapo aliyoamua kujijulisha kwa watu waliomo ulimwenguni ni kwa kuwatumia wana wa Israeli katika vizazi vyao na utaifa wao.

Mistari kadhaa inaelezea juu ya jambo hili – hatua kwa hatua: Kwanza, Mungu anataka ajulikane kwa Israeli – anaposema hivi – “Lakini sasa, Bwana aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu….nanyi ni mashahidi wangu, asema Bwana, na mtumishi niliyemchagua; mpate kujua, na kuniamini, na kufahamu ya kuwa mimi ndiye; kabla yangu hakuumbwa Mungu awaye yote, wala baada yangu mimi hatakuwepo mwingine”. (Isaya 43:1, 10)

Pili, Mungu anataka kuwatumia wana wa Israeli kujijulisha kwa ulimwengu – anaposema hivi katika Isaya 49:3 – “Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa”.

Neno hili “nitatukuzwa” lina maana ya “nitajulikana”. Kwa hiyo mstari huu tunaweza kuusoma hivi tena – “wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitajulikana”!