Bwana Yesu asifiwe sana !

Tunakusalimu katika jina la Yesu Kristo! Tunakuandikia barua hii, tukiwa hapa mjini Morogoro tukijiandaa kuanza semina leo ya siku sita!

Tunamwamini Mungu kuwa pamoja nasi katika semina hii, huku akijidhihirisha kwa kila mtu atakayekuwepo kwa kadri apendavyo – katika Roho Mtakatifu!

Kabla hatujaja hapa Morogoro, tulikuwa na semina mjini Dodoma kwa semina ya siku nane (29 mei hadi 5 juni 2016). Na siku ya alhamisi tar 2 juni 2016, tuliwahudumia wabunge na wafanyakazi wa bunge walioweza kufika kwenye “Chapel” iliyopo kwenye eneo la bunge mjini Dodoma.

Tunamshukuru Mungu sana kwa matendo makuu tuliyoyaona Mungu akiyafanya tulipokuwa Dodoma – na kwa kibali alichotupa katika mioyo ya maelfu ya watu waliokuwa wanahudhuria semina yetu kila siku.

Jukumu tunalokupa kwa mwezi huu.

Nataka liingie hili ndani ya moyo wako ya kuwa Mungu anapenda ufanikiwe, na anapenda na Yeye ashiriki katika kufanikiwa kwako huko; lakini kutumia mpango wake, alionao kwa ajili yako!

Mtazamo huu na msimamo huu wa Mungu, tunauona tunaposoma mstari wa Yeremia 29:11 usemao: “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho”.

Zipo aina nyingi za mawazo ya Mungu, zinazounda mipango aliyonayo kwa ajili yako, ili uweze kufanikiwa. Tuangalie aina ya 1 ya wazo mojawapo la Mungu, alilolikusudia kuliweka moyoni mwako, ili liweze kukujulisha na kukuongoza katika mpango wake, utakaofanikisha maisha yako.

Wazo hilo ni hili: “Ombea kwa Bwana mji unaohusika na maisha yako!”

Wazo hili linatokana na agizo la Mungu kwa wana wa Israeli alipowaambia ya kwamba: “Kautakieni amani mji ule, ambao nimewafanya mchukuliwe mateka, mkauombee kwa Bwana; kwa maana katika amani yake mji huo ninyi mtapata amani” (Yeremia 29:7).

Neno hili “amani” lililoandikwa mara tatu katika mstari huu wa Yeremia 29:7 lina maana ile ile ya neno “amani”, lililotumika katika mstari ule wa Yeremia 29:11. Neno hili “amani” lilivyotumika katika mistari hii miwili lina maana ya “mafanikio”

Ndani ya agizo lililomo katika mstari huu wa Yeremia 29:7 tunataka ujifunze na kutilia maanani yafuatayo:

  1. Kwamba; Kufanikiwa kwako katika kitu unachokifanya, kumeunganishwa na kufanikiwa kwa mji unaokaa au unaoishi. Mji ukifanikiwa kimaendeleo na wewe unatakiwa ufanikiwe vile vile! Mji ukifanikiwa kimaendeleo, wakati wewe mkaazi wake umekwama kimaendeleo, ina maana umeshindwa kupata mbinu za kujiunganisha katika mafanikio ya mji huo! “Kwa maana katika amani (mafanikio) yake mji huo ninyi mtapata amani (mafanikio)”! Haya ndiyo ambayo Mungu aliwaambia wana wa Israeli – na anakuambia na wewe pia leo!
  2. Kwamba; Ili mji unaokaa ufanikiwe kimaendeleo, unahitaji pia maombi yako. Biblia inasema: “Kautakieni amani (mafanikio) mji …mkauombee kwa Bwana” (Yeremia 29:7). Kuuombea mji kunamwonyesha Mungu haja uliyonayo moyoni mwako, ya kutaka msaada wake, ili aweze kukupa mbinu zitakazokuunganisha na mafanikio ya mji huo, ili na wewe ufanikiwe!
  3. Kwamba; Maombi unayoombea mji, yanatoa nafasi kwa Mungu “kufuatilia” aina ya maendeleo yanayoufanya mji ufanikiwe! Hii ni kwa sababu si kila mafanikio unayoyaona katika mji yanakufaa na wewe pia! Biblia inasema: “Kufanikiwa kwao wapumbavu kutawaangamiza” (Mithali 1:32)! Na Mungu asingetaka ujiunganishe na mbinu zilizopo katika mji zinazowaangamiza wanaozitumia kufanikiwa! Mbinu za mafanikio kama hizo, ndizo zinazofanya “mji” ukifanikiwa – unajikuta hautaki kumsikiliza Mungu…na wakaazi wake wanakuwa hawataki pia kumsikiliza Mungu! Mungu anasema: “Mimi nalisema nawe wakati wa kufanikiwa kwako; lakini ulisema sitaki kusikia …” (Yeremia 22:21). Mafanikio yanayokufanya usimsikilize Mungu hayakufai.
  4. Kwamba; Ukilitazama kwa mtazamo huu suala la kuombea mji ili ufanikiwe, utajikuta unaombea mji zaidi ya mmoja! Wana wa Israeli walipopewa agizo la kuombea mji wa Babeli walikuwa mbali na kwao. Na walipokuwa huko uhamishoni walijikuta wanauombea pia mji wa Yerusalemu ambako ndio kwao! Kwa hiyo ukiombea “Babeli” yako, usisahau kuombea na “Yerusalemu” yako, maana maombi ya miji inayotumika kukupa kipato chako, yanaunganisha mafanikio ya miji hiyo na kule kufanikiwa kwako!
  5. Kwamba: Hata kama mji huupendi, wewe uombee, ili kuonyesha utii wako kwa Mungu, ili akufanikishe katika kipindi ulichomo katika mji huo! Tuna uhakika wana wa Israeli hawakuupenda mji wa Babeli, lakini bado walitakiwa wauombee katika kipindi walichokuwa huko!

Semina zijazo

Ukifuatilia semina zijazo utaona ya kuwa tutakuwa sehemu zifuatazo: Tarehe 18 Juni 2016 (vijana) – Diamond Jubilee hall kwa siku moja hiyo. Tarehe 3 – 10 Julai 2016 (Mwanza mjini) kwa watu wote na tar 13 – 17 Julai 2016 (Shinyanga mjini); na tar 20 – 24 Julai 2016 (Singida Mjini).

Kongamano la maombi litakuwa tarehe 2 – 5 Agosti 2016 – siku ya kufika ni tar 1 Agosti na siku ya kuondoka ni tar 6 Agosti 2016. Na baada ya hapo tutakuwa na semina nchini Scotland kwenye mji wa Glasgow tar 12 – 14 Agosti 2016.

Mungu azidi kukubariki na tuzidi kuombeana.

Ni sisi katika utumishi wa Kristo

Christopher na Diana