Salamu katika Jina la Yesu Kristo!

Habari za Huduma: Tumeanza mwezi huu tukiwa jijini Dar es  salaam, tukiwa tunamalizia semina ya neno la Mungu. Semina hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Jangwani, tuliianza tarehe 24 februari, na tuliimaliza tarehe 3 machi 2013.

Tunamshukuru sana Mungu kwa mahudhurio makubwa yaliyokuwepo na kwa maelfu ya watu waliookoka wakati wa semina. Unaweza kuona baadhi ya picha za semina hii katika eneo hili hapa, pia sehemu ya picha katika tovuti yetu.

Tarehe 12 – 17 machi 2013 tutakuwa na semina ya neno la Mungu mjini Tanga, itakayofanyika katika uwanja wa Tangamano. Endelea kutuombea ifanikiwe sana, na kama unaweza kuhudhuria unakaribishwa.

Lakini pia semina hii tutairusha “live” kupitia tovuti yetu hii, na tovuti ya https://www.kicheko.com

Baada ya semina hii tutakuwa na mapumziko hadi semina nyingine itakayofuata tutakayokuwa nayo mjini Dodoma tarehe 21 – 28 April 2013. Pia, mwezi huu wa machi 2013, tumetoa kitabu kipya kiitwacho: “Ujue ulimwengu wa roho ili ufanikiwe katika maisha yako”.

Ni kitabu muhimu sana maana kinakupa kujua uhalisia wa ulimwengu wa roho, kwa mtazamo wa kibiblia. Unaweza kukipata katika ofisi zetu zilizopo Arusha na Dar es salaam. Na pia kitakuwa kinapatikana wakati wa semina popote tutakapokuwa.

Ujumbe wa neno kwako kwa mwezi huu:

Je, unajua umuhimu wa upako wa Roho mtakatifu katika kukuandaa uwe kiongozi? Inawezekana unajua, na inawezekana hujui; hata hivyo ujumbe huu utakupa kufikiri kwa upana zaidi, juu ya faida za upako wa Roho Mtakatifu katika maisha yako.

Mfalme Daudi alipakwa mafuta ya Roho Mtakatifu mara tatu katika maisha yake. Daudi alipokuwa mjini Bethlehemu, alipakwa mafuta hayo kwa mara ya kwanza.

“Ndipo samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia  mafuta kati ya ndugu zake; na Roho ya Bwana akamshukia Daudi kwa nguvu tangu siku ile” (1Samweli 16:13).

 Tunajua pia kwa kusoma Biblia ya kuwa, Daudi alipakwa mafuta mara ya pili (2 Samweli 2:4), na mara ya tatu (2 Samweli 5:3), akiwa mjini Hebroni.