Salamu Katika Jina la Yesu Kristo.

Tunakuandikia barua hii tukijua ya kuwa neema ya Mungu iko juu yako, ili kuendelea kutupa  mkono wa shirika katika utumishi huu ambao Mungu ametupa katika nyakati hizi.

Semina Tulizokwishafanya

Semina tulizozifanya mwezi wa Februari 2014, ni tatu. Tulifanya Moshi mjini tarehe 28 Januari hadi tarehe 2 Februari. Halafu tukawa na semina nyingine Arusha mjini tarehe 9 – 16 Februari 2014. Baada ya kumaliza semina ya mjini Arusha, tulielekea Dar es salaamu, ambako tulifanya Semina tarehe 23 Februari hadi tarehe 2 Machi 2014.

Tunawaandikia barua hii, leo tarehe 20 Machi 2014 – baada ya kumaliza semina tuliyokuwa nayo Tanga tarehe 11 – 16 Machi 2014.

Tunamshukuru Mungu sana kwa mahudhurio mazuri ya watu waliofika kushiriki semina hizi zote. Ingawa wakati mwingine palikuwa panatokea mvua, lakini hata hivyo mvua hizo hazikuzuia watu kufika kwenye semina!

Matukio.

Matukio mengi sana muhimu yaliyojitokeza tulipokuwa tunafanya semina nilizozitaja hapo juu. Hatutaweza kuyaandika yote, bali tutakushirikisha baadhi tu – kama ifuatavyo:

Mungu alitupa tena neema ya kutumia redio na mtandao wa intaneti katika kurusha ‘live’ matangazo ya semina hizi.

Kwenye mtandao wa intaneti tulikuwa tunarusha kupitia www.mwakasege.org na www.kicheko.com. Kwa upande wa redio – kwa semina zote tatu, redio sauti ya injili (Kutoka Moshi mjini) na redio HHC Alive (Kutoka Mwanza mjini) zilikuwa hewani. Ila kwa semina ya Arusha, tuliongeza redio Safina ya Arusha, na Semina ya Dar tuliongeza redio Wapo na redio Upendo zote za Dar es salaamu.