Bwana Yesu asifiwe sana!

Unaendeleaje na maisha mwana wa Mungu? Sisi tunaendelea vizuri. Mwezi wa Februari tarehe 16 – 21, tulifanya semina mjini Moshi, na tuliuona ukuu wa Mungu katika mafundisho na katika udhihirisho wa nguvu zake. Pia – hadi mwisho wa semina watu wapya waliookoka katika semina hiyo walifika elfu saba (7000)!

Katika barua ya mwezi huu tunataka ufahamu mambo yafuatayo – na ikiwa unayafahamu basi kwa barua hii Mungu akukumbushe juu ya umuhimu wake.

Jambo la 1: Wewe ni balozi wa Kristo na kwa ajili ya Kristo hapa ulimwenguni. Hii ni kwa sababu Biblia inasema: “Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu” (2 Wakorintho 5:20). Tafsiri nyingine ya neno hili “wajumbe” maana yake “mabalozi”

Jambo la 2: Ikiwa wewe ni balozi, basi wewe si wa ulimwengu huu kama vile Kristo asivyo wa ulimwengu huu, ingawa kwa sasa unaishi katika ulimwengu huu. Hii ni kwa sababu Yesu alipokuwa anatuombea ulinzi kwetu sisi watu wake tuliopo duniani alimwambia Baba yake aliye mbinguni, ambaye ni Baba yetu pia ya kuwa: “Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu” (Yohana 17:16).

Jambo la 3: Ikiwa wewe si wa ulimwengu huu, kama Yesu asivyo wa ulimwengu huu, ina maana na wewe umetumwa kama Kristo alivyokuwa ametumwa. Hii ni kwa sababu Yesu alimwambia Mungu katika maombi juu yetu hivi: “Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni” (Yohana 17:18).

Jambo la 4: Ikiwa wewe umetumwa hapa ulimwenguni kama Yesu alivyotumwa, ina maana umetumwa uwe mwakilishi wa Mungu katika Neno lake; kama vile Yesu alivyokuwa Neno, lakini akafanyika mwili; ili awe mwakilishi wa Mungu katika Neno – hapa ulimwenguni.

Jambo la 5: Kama vile ambavyo Yesu hakutumwa hapa ulimwenguni peke yake, ndivyo na wewe hujaachwa hapa ulimwenguni peke yako baada ya kuokoka kwako. Yesu akiwa hapa ulimwenguni, alifanya kazi na Mungu kwa njia ya neno lake na kwa Roho wake Mtakatifu. Na wewe unatakiwa ufanye kazi hapa ulimwenguni pamoja na Mungu – kwa njia ya neno lake na kwa Roho wake Mtakatifu. Kwa maana imeandikwa: “Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na Mungu, ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu” (1 Wakorintho 3:9).

Jambo la 6: Tunataka ujue ya kuwa agenda mojawapo kubwa tuliyonayo ya kukuombea mwezi huu, ni Mungu aongeze ndani yako kiwango chako cha utendaji wa Neno lake, kwa uongozi wa Roho mtakatifu – ili uzidi kufanikiwa katika kuwa mwakilishi wake hapo ulipo – na kila mahali utakapokuwa.

Semina

Mwezi huu tuna semina jijini Dar, itakayofanyika tarehe 6 – 13, kwenye viwanja vya michezo vya Chuo kikuu cha Dar es salaam (UDSM), kila siku jioni kuanzia saa 10 jioni. Karibu kwenye semina, na tafadhali mshirikishe na mtu mwingine juu ya hili. Mungu azidi kukubariki kwa kusimama pamoja nasi katika kumtumikia Mungu mwaka huu.

Tuzidi kuombeana.
Ni sisi katika utumishi wa Kristo
Christopher na Diana Mwakasege.