Salamu katika jina la Yesu Kristo!

Tunashukuru ya kuwa Mungu amekupa nafasi ya kuisoma barua yetu hii ya mwezi huu.

Mwezi uliopita wa Aprili, tarehe 21 hadi 28 tulikuwa na semina ya neno la Mungu mjini Dodoma. Semina hiyo ilifanyika katika uwanja wa Barafu, ndani ya hema tunalosafiri nalo kwa ajili ya semina hizi.

Na siku ya jumamosi tarehe 27 April asubuhi, tulipata nafasi ya kuwa na semina maalum ya vijana iliyohusu masuala ya Fikra za kiuongozi.

Tunamshukuru Mungu sana kwa ushindi mkubwa aliojitwalia Bwana Yesu kwa ajili ya ufalme wake katika semina hiyo.

Tarehe 1 – 5 Mei tulikuwa na semina mjini Singida, iliyofanyika katika uwanja wa ‘Peoples’. Tulimwona Bwana Yesu akijifunua kwa namna ya ukuu sana katika semina ya mwaka huu, kuliko semina tuliyofanya mwaka jana eneo hilo hilo.

Pia tuliweza kuwa na vijana tarehe 4 asubuhi kwa ajili ya mafundisho juu ya fikra za kiuongozi. Maelfu ya vijana walihudhuria.

Tulipokuwa Dodoma na Singida tulipata nafasi ya kujifunza kwa undani juu ya sehemu ya imani katika kumkutanisha mwanadamu na uwepo wa Mungu, wakati anapotoa sadaka.

Ndani ya barua hii tunataka tukukumbushe mambo mawili makubwa; 1: Juu ya tabia ya Imani; na 2: Juu ya kuiweka imani mahali inapostahili.

Jambo la kwanza : Tabia ya imani

Kwa mtu yeyote aliyefuatilia kwa karibu juu ya somo la imani, atakuwa amegundua ya kuwa imani ina tabia yake. Kama unalijua hili basi ni vizuri sana na upo mahali pazuri. Lakini ikiwa ulikuwa hujui basi ngoja tukupe mifano michache.

  • Imani inaweza kuongezeka. Wanafunzi walimwambia Yesu awaongezee imani (Luka 17:5). Kama imani inaweza kuongezeka, basi inaweza kupungua pia!
  • Imani ina ngazi (levels) mbali mbali. Biblia inasema juu ya “…toka imani hata imani” (Warumi 1:17)