Jina la Yesu litukuzwe milele!

Jizoeze kujifunika kwa damu ya Yesu ili ikukinge na

  1. Adhabu ya Mungu
  2. Kisasi cha shetani juu yako

Biblia inatuambia ya kuwa Yesu Kristo ndiye “Pasaka” wetu. Hii ni kwa sababu imeandikwa ya kuwa: “Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa sadaka, yaani, Kristo” (1Wakorintho 5:7)

Yesu Kristo alipokufa msalabani, alifanyika sadaka iitwayo Pasaka! Jambo hili linatupa uhalali sisi tunaomwamini Kristo Yesu, kama Bwana na Mwokozi wetu, kuitumia damu ya Yesu, kama vile damu ya Kondoo aliyeitwa Pasaka ilivyotumika na wana wa Israeli.

Tunataka tukutie moyo juu ya wewe kujua ya kuwa una uhalali katika Kristo Yesu, kuitumia damu yake – kama damu ya Sadaka iitwayo Pasaka.

Unaposoma kitabu cha Kutoka sura ya 12 utaona ya kuwa Mungu alimwagiza Musa juu ya utoaji huu wa sadaka ya Pasaka, na akampa maagizo ya namna ya kuitumia damu ya Pasaka; na akamweleza faida ambazo wangezipata ikiwa wangeitumia ile damu ya Pasaka, kama alivyokuwa anawaaagiza!

 Agizo walilopewa la kuchukua “baadhi ya damu yake na kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti” cha milango ya nyumba zao; ilikuwa ni ishara ya KUJIFUNIKA kwa damu ya Pasaka.

Sababu mojawapo ya kutaka wafanye hivyo ni ili pigo la Mungu au adhabu ya Mungu lisiwapate.

Mungu alisema:

“Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri….Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lolote likawaharibu, nitakapopiga nchi ya Misri” (Kutoka 12: 12, 13).

Tunapoendelea kuisoma habari hii, tunaona ya kuwa, kila nyumba iliyokuwa imefunikwa kwa damu ya Pasaka, ilikaa katika kinga ambayo ilizuia pigo la Mungu lisiwapate wale wa nyumba husika.