Bwana Yesu asifiwe sana!

Tunakuandikia barua hii ya mwezi huu tukitamani moyoni mwetu, uungane nasi katika kuibariki nchi ya Israeli na raia wake. Tarehe 14 mei 1948 nchi ya Israeli ilizaliwa, nasi katika kumbukumbu hii, tumeona tutumie nafasi hii kukutaka uwe unajizoeza kuibariki Israeli.

Mwaka 2007 mwezi wa Desemba, tukiwa nchini Israel, Mungu alisema nasi juu ya kuwahimiza watu wake wajiunganishe na nchi ya Israel Kibiblia.
Na kwa kufanya hivyo watakuwa wanaibariki nchi ya Israel, kama sehemu ya maagizo ambayo Mungu amewapa watu wake ulimwengu mzima.

Agizo hili lilikuwa ni sehemu ya hatua mojawapo muhimu katika kupanuka kwa huduma ambayo Mungu ametupa katika nchi ya Tanzania, na nchi nyingine ulimwenguni. Hii ndiyo sababu ya kukutaka uungane nasi katika kuibariki nchi ya Israeli. Tunajua ya kuwa hakuna mtu anayeibariki nchi ya Israeli, naye asibarikiwe na Mungu wa Ibrahimu, Isaka na wa Yakobo (Israeli).

Mungu aliahidi jambo hili katika kitabu cha Mwanzo 12:3 alipomwambia Ibrahimu ya kuwa: “….Nitawabariki wakubarikio….Na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa”. Unaweza kuungana nasi katika kuibariki Israeli kwa njia zifuatazo:

1. OMBEA NCHI YA ISRAELI
Nchi ya Israeli haipo pale kama nchi kwa ajili ya raia wake tu, na kwa watu waishio ndani yake tu; lakini iko pale ili Mungu aitumie kwa ajili ya kujijulisha na kuwafikia watu wote ulimwenguni. Kumbuka ya kuwa Mungu anaitumia nchi ya Israel kama Lango la kupitisha yale yote aliyokusudia uyapate kutokana na agano lake alilolifanya na Ibrahimu. Unapoiombea Israeli – Mungu anailinda na kuitunza ili itumike kupitisha vitu ambavyo Mungu anataka vikufikie.

2. OMBEA MJI WA YERUSALEMU
Kufuatana na Ezekiel 26:2; “Yerusalemu” ni “lango la kabila za watu”. Tena kufuatana na Mathayo 5:35; “Yerusalemu” ni “mji wa mfalme mkuu” …yaani Yesu Kristo! Ikiwa umeungwa kwa Kristo Yesu, basi mji huu wa Yerusalemu unakuhusu sana! Ni lango la Mungu kwa ajili ya kabila za watu – na wewe ukiwa mmojawapo! Ndiyo maana katika Zaburi 122:6 tunahimizwa kuuombea mji huu amani na kuupenda!

3. UWE NA BENDERA YA ISRAELI
Jitahidi uwe na bendera kadhaa za nchi ya Israel. Halafu ziweke au zipeperushe ofisini kwako, au sehemu yako ya biashara, au nyumbani kwako, au mahali pengine panapokuhusu wewe binafsi kama vile Roho Mtakatifu atakavyokuongoza. Hii itakuwa nafasi ya kueleza uhusiano wako na taifa la Israeli kama uzao wa Ibrahimu kwa Imani uliyonayo katika Kristo Yesu. Hii ni sawa na mstari wa Wagalatia 3:29 usemao: “Na kama ninyi ni wa Kristo,basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi”

4. FUTA LAANA DHIDI YA NCHI YA ISRAELI ZILIZOTAMKWA KUTOKEA TANZANIA.
Mungu alimwambia Ibrahimu ya kuwa: “…Akulaaniye nitamlaani…” (Mwanzo 12:3) kumbuka ya kuwa kuwepo kwa taifa la Israeli ni tunda mojawapo la agano kati ya Mungu na Ibrahimu. Kwa hiyo unaposikia mtu yeyote ambaye ni mtanzania anailaani nchi ya Israeli; au si mtanzania lakini anailaani Israeli akiwa katika nchi ya Tanzania – usikae kimya! Unayo mamlaka katika jina la Yesu kutumia Damu ya Yesu (i) kuomba toba kwa ajili ya, na kwa niaba ya Tanzania kwa ajili ya laana hiyo dhidi ya nchi ya Israeli; (ii) kuomba maombi ya kuifuta laana hiyo, na badala yake achilia maneno ya kuibariki nchi ya Israeli.       5.  

MUELIMISHE MWINGINE JUU YA KUTAFSIRI MAMBO YA ISRAELI KIBIBLIA
Watu wengi wanaposikia habari ya nchi ya Israeli na mambo yanayotokea katika nchi hiyo, wanayatafsiri kisiasa au kidini. Ukitafsiri mambo ya nchi ya Israeli kidini au kisiasa huwezi kuyaelewa kwa jinsi yanavyotakiwa kueleweka.

Nchi ya Israeli haikuzaliwa kisiasa au kidini – ingawa Umoja wa Mataifa ulitumika ili kutengeneza mazingira ya kuzaliwa kwake tarehe 14 mei 1948.

Mungu anasema juu ya Israeli katika Isaya 44:21: “Nawe Israeli, wewe u mtumishi wangu; nimekuumba, u mtumishi wangu; Ee Israeli, hutasahauliwa na mimi”  
Na Mungu alimtumia Farao ujumbe kupitia kwa Musa ajue ya kuwa; “Israeli ni mwanangu mimi, mzaliwa wa kwanza wangu…” (Kutoka 4:22,23).

Hii lugha ya Mungu haieleweki na watu wanaotaka kutafsiri mambo ya Israeli kisiasa au kidini… na kwa sababu hii hawaelewi wanavyotakiwa kuelewa juu ya kwa nini mambo yanatokea yanavyotokea katika nchi ya Israeli, kwa jinsi yanavyotokea.

Ni jukumu lako kuibariki nchi ya Israeli kwa kumuelimisha mtu mwingine umuhimu wa kutafsiri mambo ya Israeli kwa jicho la Biblia.

6. SAFIRI PAMOJA NASI KWENDA ISRAELI
Tokea mwaka 2007 tumekuwa tukifanya safari zisizopungua mbili au tatu kila mwaka za kuitembelea nchi ya Israeli kwa malengo ya kiroho.
Unaposoma katika biblia sehemu mbalimbali, hutakosa kuona ya kuwa Mungu aliahidi kuibariki nchi ya Israeli kwa kuwaleta watu toka mataifa mbalimbali kuitembelea nchi hiyo. Kwa hiyo unapoitembelea nchi ya Israeli unaibariki nchi hiyo. Kumbuka ukiibariki Israeli,na Mungu wa Ibrahimu anakubariki na wewe pia.
Pamoja na kusafiri wewe binafsi, unaweza pia kusafiri kwa njia ya kutoa sadaka ya kumsafirisha mtu mwingine.

7. TOA SADAKA KUTUSAIDIA NA KUTUOMBEA ILI HUDUMA TULIYO NAYO KUHUSU ISRAELI IWEZE KUFANIKIWA ZAIDI
Safari yetu ya kwanza ya kuitembelea nchi ya Israeli mwezi mei 2007 ilimalizika kwa washiriki kuunda familia ya MANA juu ya safari za Israeli. Lengo lake likiwa ni
(i) Kukutana mara kwa mara kutuombea tufanikiwe katika huduma hii;
(ii) Kuanzisha mfuko maalum wa sadaka ambao watu watakuwa wanaweka sadaka ya fedha ili kufanikisha huduma hii ya kuunganisha watu wa Mungu na Israeli.

Unaweza na wewe ukawa mmoja wa familia hii ya MANA – Israeli kwa njia ya kutuombea na kutoa sadaka katika mfuko huu.
Kumbuka “Baraka ya Ibrahimu” inakuhusu wewe na UZAO WAKO. Kwa hiyo kumbuka kutoa sadaka pia kwa ajili ya kuunganisha watoto (na wajukuu wako kama unao) na nchi ya Israeli.

Semina zilizopo mwezi huu ni 6 – 8 mei 2016 kule Columbus, OHIO nchini Marekani na tarehe 29 mei – 5 Juni 2016 mjini Dodoma, Tanzania.

Tuzidi kuombeana
Christopher na Diana Mwakasege.