Salamu katika jina la Yesu Kristo!

Huu ni mwezi wa Novemba, ikiwa ni ishara muhimu ya kuwa mwezi ujao wa Disemba, ndio mwezi wa mwisho kwa mwaka huu wa 2013!

Je, umekumbuka kutoa sadaka ya shukrani, kwa Mungu kukuvusha salama, na kwa ushindi, katika “msimu” uliopita wa mtiririko wa maisha yako?

Je, unaijua gharama unayoweza kupata kwa kutokutoa sadaka ya shukrani kwa Mungu, kwa jinsi alivyokusaidia katika kipindi kilichopita cha maisha yako? Gharama unayoweza kuipata ni hii: Mungu kukuacha ukaingia, na kuanza kuishi katika kipindi kipya cha maisha yako, bila msaada wa maelekezo toka kwake, juu ya namna unavyotakiwa kuishi na kuenenda.

Gharama ya jinsi hii, iliwahi kumpata nabii Musa baada ya kuvuka bahari ya Shamu (Kutoka Sura ya 14), na kabla hajafika mlima Sinai (Kutoka Sura ya 19). Ni dhahiri ya kuwa katika kutoka sura ya 15, tunaona wakimwimbia Mungu juu ya ushindi ambao aliwapa dhidi ya Farao na Wamisri; lakini hatuoni wakitoa sadaka ya shukrani kwa ajili ya jambo hilo.

Hili jambo ni muhimu kwa sababu, kutokana na Zaburi 50:23, unapotoa sadaka ya shukrani, sii tu kwamba Mungu anajua unamshukuru kwa mambo aliyokutendea, lakini pia anajua ya kuwa kwa sadaka hiyo unampa fursa nyingine ya kujitukuza katika kipindi cha maisha kilichoko mbele yako. Zaburi 50:23 inasema hivi:

"Atoaye sadaka za kushukuru, ndiye anayenitukuza. Naye autengenezaye mwenendo wake, Nitamwonyesha wokovu wa Mungu."

Biblia inaposema sadaka yako ya shukrani inamtukuza Mungu, ina maana inampa Mungu nafasi ya kuendelea kujitukuza katika maisha ya mtoa sadaka. Mungu atajitukuza vipi kwa mtoa sadaka? Mungu atajitukuza kwa kumpa maelekezo ya namna ya kuishi kwa ushindi, na kwa mafanikio katika maisha yaliyo mbele ya mtoa sadaka! Na watu watakapokuwa wanaangalia maisha ya mtoa sadaka – watajua ya kuwa Mungu yu pamoja naye katika maisha yake!

Musa alijikuta yupo katika msimu mpya wa maisha, na msimu mpya wa huduma; - na akayaendesha maisha, na akaiendesha huduma, kama yeye alivyoona vema.