Bwana Yesu Asifiwe milele!

Ni furaha yetu katika Roho Mtakatifu kupata nafasi ya kuwasiliana na wewe kwa njia ya barua hii.

Mungu ni Mwema; tena ni Mwaminifu, kwa kila amtegemeaye katika maisha yake ya kila siku. Sisi tumeuona tena wema huo, na uaminifu huo katika yale tuliyoyaona Mungu akiyafanya katika huduma aliyotupa kuifanya mwezi uliopita, yaani mwezi wa Septemba.

Tulikuwa na semina jijini Dar es salaam, katika uwanja wa Jangwani tarehe 8 – 15 Septemba. Semina hiyo ilikuwa inafanyika kila siku katika tarehe hizo kuanzia saa 10 hadi 12 jioni.

Siku ya jumamosi asubuhi, tarehe 14 Septemba, tulifanya semina ya vijana juu ya uongozi. Ingawa semina ililenga vijana, tuliwakaribisha pia watu wazima waliotaka kusikia somo hilo waweze kuhudhuria.

Tunamshukuru Mungu sana kwa mahudhurio makubwa tuliyoyaona siku zote za semina hiyo. Na pia tunamshukuru Mungu kwa maelfu ya watu waliookoka katika kipindi hicho. Semina ya watu wote waliokoka jumla ya watu 2222 kwa siku zote nane. Na kwenye semina ya vijana, waliokoka watu 503.

Tunaamini utazidi kuungana nasi katika kumshukuru Mungu juu ya mavuno hayo ya roho za watu kwa ajili ya ufalme wa Mbinguni. Na tena tuwaombee wapate kukua katika kumjua Yesu Kristo; na wakue katika neema yake; na wapate kuukulia wokovu – bila kupoa wala kurudi nyuma!

Unaweza kuangalia baadhi ya picha za semina hiyo hapa. Siku ya mwisho ya semina tulipata mahudhurio makubwa sana ambayo hatukuwa tumewahi kuyaona kwenye semina zetu zingine, tulizowahi kuzifanya jijini Dar.

Tulishuhudia pia kwa macho yetu, na kusikia kwa masikio yetu, Mungu akiwaponya watu magonjwa yaliyokuwa yanawasumbua.

Glory be to God in the Highest!