Shaloom!

Bwana Yesu Kristo asifiwe!

Tunaamini Mungu anakutunza na unaendelea vizuri na majukumu yako ya kila siku.

Sisi tunaendelea vizuri na kazi ya Mungu aliyotukabidhi katika kizazi hiki. Mwezi uliopita, yaani mwezi wa Agosti, ulikuwa na ratiba ambayo ilikuwa imebana sana.

Tulikuwa na Semina mjini Shinyanga tuliyoifanya tarehe 31 julai hadi tarehe 4 Agosti. Semina hiyo tuliifanya ndani ya hema, katika uwanja wa Kambarage.

Baada ya Shinyanga, tulielekea mjini Tabora, ambako tulikuwa na semina ya siku 4 – tarehe 8 – 11 Agosti 2013. Semina hiyo tuliyoifanya ndani ya hema, ilikuwa na mafanikio makubwa sana, licha ya kwamba ilifanyika kipindi hicho hicho ambacho Waislamu walikuwa na Sikukuu yao ya Iddi kitaifa mjini Tabora.

Tarehe 15 – 18 Agosti 2013, tukawa na semina Kigoma mjini. Kigoma hatukuenda na hema letu tunalotumia kufanyia semina, kwa sababu barabara siyo nzuri. Kanisa la Kiangilikana mjini Kigoma – lililopo eneo la Mwanga, walitupa nafasi ya kutumia jengo lao la Kanisa kufanyia semina yetu.

Tunakusihi ushirikiane nasi kuombea usafiri katika mikoa ya Tabora na Kigoma. Barabara za Nzega hadi Tabora mjini, halafu ile ya Tabora mjini hadi Kigoma mjini kupitia Uvinza, zinatakiwa zijengwe hadi kufikia kiwango cha lami, lakini ujenzi huo unakwenda polepole sana. Hebu tuombe ujenzi huu uharakishwe na kufikia kiwango kizuri na imara cha lami. Mwaka ujao (2014), tunataka Mungu akitupa nafasi ya kwenda Kigoma, tuende na hema letu la kufanyia Semina. Pia, Ombea usafiri wa ndege, maana hauko vizuri kama inavyotakiwa katika mikoa hiyo miwili.

Baada ya Kigoma, tulirudi Arusha mjini kwa ajili ya kufanya semina ya pili kwa mwaka huu. Semina hiyo tuliyoifanya katika kiwanja cha reli, tuliifanya tarehe 25 Agosti hadi tarehe 1 Septemba 2013. Ilikuwa ni Semina iliyokuwa na mahudhurio makubwa sana kwa siku zote nane!

Ili kupanua wigo wa semina hizi, pia tulikuwa tunarusha ‘live’ kwenye redio mbalimbali na pia kupitia mtandao wa Intaneti. Tukiwa Tabora tulimshukuru Mungu sana, pale alipotupa kibali kwa redio inayomilikiwa na mwislamu, kukubali kurusha semina ‘live’ kwa wasikilizaji wake!