Inaendelea……………

3. SAMEHE NA KUSAHAU:
Wakati fulani nilikuwa mahali nikifanya semina ya neno la Mungu. Mtu mmoja akanifuata na akaniambia anataka nimuombee.
Nikamuuliza; “Nikuombee nini?” Akasema;  “Mimi shida yangu ni kwamba naona imani yangu ni ndogo na haikui, na maombi yangu hayajibiwi. Kwa hiyo naona nina shida katika maisha yangu ya kiroho, uniombee“.

Inawezekana hata wewe una shida ya namna hiyo, kwa hiyo tafakari kwa makini maneno haya.
Niliahidi kumuombea baadaye kwa maana muda ulikuwa umekwisha.
Siku moja nilipokuwa ninaomba kwa Mungu juu ya shida yake, Bwana akanijibu katika roho yangu kuwa:
“Mtu huyo ana matatizo ya ndoa na kuna jambo lililomuudhi. Yeye anafikiri amesamehe, lakini bado ana uchungu moyoni mwake. Mwambie asamehe na kusahau na shida yake itakwisha”.

Nilipowasiliana naye juu ya jambo hili, alikubali kuwa, ni kweli mwenzie amekuwa akimkosea mara kwa mara katika ndoa yao. Lakini alisema amekwisha msamehe.
Nikamuuliza; “Je! mbona basi kila mkikosana unakumbusha makosa ya nyuma?”
Akajibu; “Ni kweli, sasa nifanyeje wakati naona kila wakati makosa aliyonifanyia nyuma yakinijia kichwani?”
Hili ni tatizo la wengi. Na hujikuta wanasema wamesamehe kumbe bado. Msamaha si jambo la akili ni hatua ya rohoni. Ni uamuzi unaotoka ndani ya moyo wako.

Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, sikuambiii hata mara saba, bali hata saba mara sabini” (Mathayo 18:21, 22)

Na kama akikukosea mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba , akisema, nimetubu msamehe. Mitume wakamwambia Bwana tuongezee imani” (Luka 17:4,5).

Mistari hii inatuonyesha jinsi kukua kwa imani, kunavyohusiana sana na kusamehe.
Wanafunzi walimwambia Bwana Yesu, awaongezee imani. Kwa kuwa walifahamu kwamba, kwa uwezo wao wasingeweza kusamehe kama Kristo anavyotaka.
Ni kweli kabisa.
Kama vile unavyohitaji imani katika kuomba, vile vile katika kusamehe na kusahau unahitaji imani.

Ulipompokea Kristo ulipokea kiasi cha imani (Warumi 12:3)
Na ili iongezeke unahitaji kusoma neno la Mungu na kulitenda. Imani huja kwa kusikia Neno la Mungu. (Warumi 10:17).
Imani ni ya rohoni na kusamehe ni kwa rohoni.
Unawezaje kusamehe na usiyakumbuke uliyofanyiwa?

Hilo ndilo tatizo kubwa alilokuwa nalo yule mtu aliyeniambia niomuombee. Na wengi pia wana tatizo la namna hii, na limekwamisha uponyaji na majibu mengine ya maombi yao, wameombewa mara nyingi, lakini bila mafanikio.
Kusamehe na kusahau ni kitendo cha imani ambacho ni budi kionekane kwa njia ya matendo ya mtu.

Kusamehe ni uamuzi wa mara moja na kusahau ni vita vya imani.
Sasa, utaniuliza, Ndugu Mwakasege, utawezaje namna hiyo?
Kabla sijakujibu, na mimi nakuuliza swali.
Siku ulipotubu dhambi zako, ulikuwa na uhakika gani ya kuwa Mungu amekusamehe wala hazikumbuki dhambi zako tena?
Utasema kwa kuwa ukitubu Mungu anasamehe.

Ni sawa kabisa. Hata mimi nakubaliana na hilo.
Lakini, je! Unaona kuwa Mungu anaweza kukuambia ufanye kitu ambacho anajua huwezi kukifanya?
Hapana hata kidogo. Bwana wetu si dhalimu!

Anafahamu kuwa WEWE MWENYEWE HUWEZI, LAKINI YEYE KWA KUWA YUMO NDANI YAKO ATAKUWEZESHA KUSAMEHE NA KUSAHAU.
Unayaweza yote katika yeye akutiaye nguvu (Wafilipi 4:13)
Ukiisha amua kumsamehe mtu hakikisha kwamba hulisemi tena jambo hilo katika kinywa chako.

Kumbuka kinywa kinanena yaujazayo moyo (Mathayo 12:34)
Na hayo maneno ndiyo yamtiayo mtu unajisi (Mathayo 15:18 – 20)
Usitafakari wakati wo wote ule, kosa ulilofanyiwa; mawazo mabaya yanapokujia juu ya kosa ulilofanyiwa, fahamu kuwa ni shetani na nafsi yako tu.
Biblia inasema mpingeni shetani naye atawakimbia (Yakobo 4:7)
Na wala msimpe nafasi (Waefeso 4:27)

Mwambie shetani aondoke na mawazo yake, kwa kuwa hilo kosa umelisamehe na kulisahau.
Na wakati huo utafakari nini?
Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote ya kupendeza, yo yote yenye sifa njema, ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, YATAFAKARINI YAYO” (Wafilipi 4:8)

Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili; bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha MAWAZO na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na TUKITEKA NYARA KILA FIKRA ipate kumtii Kristo” (2 Wakorintho 10:3 – 5)

Kusahau ni vita vikali vya imani vinavyopiganwa katika mawazo yako. Unaposhinda vita hivi, unajikuta umepiga hatua kubwa ya imani!
KWA HIYO KUMBUKA: Unasamehe kwa ajili yako Mwenyewe.
Na unasahau makosa uliyokosewa kwa ajili yako mwenyewe.

Kumbuka hili kila wakati, unamsamehe aliyekukosea na kuyasahau aliyokukosea kwa ajili yako mwenyewe.
Na kila wakati wazo likija kukukumbusha kosa hilo likatae kwa Jina la Yesu. Na USIKUBALI KULISEMA TENA MAISHANI MWAKO.

4. HASIRA IPELEKE KWENYE MAOMBI:
Mwe na hasira, ila msitende dhambi jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; wala msimpe Ibilisi nafasi” (Waefeso 4:26, 27)

Mwe na hasira, ila msitende dhambi, ni mstari ambao watu wengi wameutumia vibaya. Kutokana na maneno hayo wamefanya vitendo vingi viovu kwa mawazo, maneno na kwa matendo.

Biblia haiwezi kujipinga yenyewe. Roho Mtakatifu ndiye aliyewaongoza watu kuandika maandiko hayo Matakatifu.
Lakini, soma mistari ifuatayo:
Uchungu wote na ghadhabu na HASIRA na kelele na matukano YAONDOKE KWENU” (Waefeso 4:31)

“….. HASIRA ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu” (Yakobo 1:20)
“Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya HASIRA watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu” (Wagalatia 5:19 -21)
Hapa unaona jinsi hasira ilivyofananishwa na uchawi, uasherati, uadui, ibada ya sanamu, na mambo mengine kama hayo ambayo yanamzuia mtu asiurithi ufalme wa Mungu.

Na Yesu Kristo akikaza ubaya wa hasira alisema:
Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue; na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni, kila amwoneaye ndugu yake HASIRA itampasa HUKUMU” (Mathayo 5:21, 22)

Yesu anasema ukiwa na hasira unastahili hukumu, lakini Roho aliyesema ndani ya Kristo, ni huyo huyo aliyesema ndani ya Paulo kuwa, “Mwe na hasira, ila msitende dhambi”.

Je! Unafikiri biblia inagongana yenyewe? Hapana! Paulo alikuwa ana maana gani aliposema tuwe na hasira lakini tusitende dhambi? Unawezaje mtu ukawa na hasira lakini usitende dhambi?

Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya magonjwa na hasira.
Ngoja nikueleze jinsi mimi yalivyonitokea.
Mara tu mimi nilipompokea Kristo katika roho yangu, kulikuwa na kitu kimoja kilichokuwa kikinisumbua. Ilikuwa mtu akiniudhi nilikuwa nakasirika haraka sana. Na wakati wote nitakuwa nalifikiria jambo hilo moyoni mwangu.

Mwisho wake nilikuwa naona uchungu unaingia moyoni mwangu.
Sasa kila mara nilipokasirika nilikuwa nashindwa kuomba na mara ninaanza kuumwa homa.Jambohili lilinisumbua muda mrefu. Kila nikitubu na kumsamehe aliyenikosea, na kuliacha hilo mikononi mwa Mungu; ugonjwa niliokuwa nao ulikuwa unapona.

Nilifahamu kitu kimoja kuwa nikiweza kulitatua tatizo la hasira, ugonjwa huo hautaniruida tena. Kwa kuwa ulikuwa unakuja mara tu nikikasirika.
Nikawa na tatizo la hasira mikononi mwangu.
Kwa hiyo, nikamlilia Mungu katika maombi juu ya shida hii.

Watu wengi wanatatizo la namna hii, kila wanapokasirika juu ya jambo fulani, wanaugua. Utakuta wengi wakikasirika wanaumwa vichwa, vidonda vya tumbo, kifua, moyo, damu kwenda mbio, homa, na magonjwa mengine.
Tatizo si ugonjwa hapo. Tatizo ni hasira!

Nilipokuwa nikiomba, Roho wa Bwana alinipa jibu na naamini kuwa kama nilivyosaidiwa mimi na wewe utapata msaada. Na ndiyo maana nimekushirikisha hili.
Unapoona kuwa kuna jambo limekuudhi, usiwe mwepesi kujibu au kufanya kitu. Tulia kimya na tafuta nafasi uanze kuomba.

Kwanza tubu kwa Baba juu ya kukasirika kwako, na pili, mwambie Baba jinsi unavyojisikia moyoni mwako, bila kumficha kitu, na tatu, mwombe kitu ambacho unataka akufanyie katika jambo hilo.

Utajikuta unapoomba na kuumimina moyo wako kwa Bwana, Yeye ataichukua hiyo hasira uliyokuwa nayo na uchungu wote. Na badala yake anahuisha upya upendo mpya ndani ya moyo wako utakaokuwezesha kupita juu ya tatizo ulilo nalo. Ukiona bado hasira inatokea, ikemee kwa jina la Yesu, na itatoweka.
Paulo aliposema, Mwe na hasira, ila msitende dhambi hakuhalalisha ya kuwa hasira ni nzuri.

Kwa maneno mengine alikuwa akisema kuwa unapopata uchungu kwa kuudhiwa angalia usifanye vitendo vitakavyomuaibisha Kristo.
Kwa kuwa kuudhiwa kupo maadamu upo duniani, na kwa mtu wa Mungu maudhi yanazidi. Lakini Paulo anasema watu wajue namna ya kuishughulikia hasira inapokuja kutokana na maudhi.

Ndiyo maana aliendelea kusema:
Jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka, wala msimpe ibilisi nafasi” (Waefeso 4:26,28)

Usimpe ibilisi nafasi kwa kuiacha hasira ikazaa ugomvi, matusi na fitina.
Uchungu huo utautoaje?
Usiupeleke kwa aliyekuudhi, wala usikae nao. Upeleke kwenye maombi na upendo utavuma baada ya Mungu kuondoa uchungu uliokuwa nao.
Kuna wengine wanasema hasira aliyonayo ni ya ukoo kwa kuwa ndugu zake waliomtangulia wana hasira.

Kuna wengine huwa wakikasirika kuna kitu kinapanda na kikifika shingoni kinamfunga asiseme, na anaanza kupumua kwa nguvu na wakati mwingine huanza kulia.

Ukiona namna hiyo, chukua silaha mkononi ya Jina la Yesu na ukemee. Maana hiyo ni roho ya shetani iliyojifunika katika hasira.
Hakuna hasira ya ukoo kwa watu wa Mungu, ambao ni uzao mpya katika uzao wa Mungu. Ukoo wako ni ukoo wa Mungu. Ni ukoo wa Upendo si wahasira.
Baada ya mimi kuchukua hatua hizo, ule ugonjwa sijauona tena, na hasira sikuiona kunifuatafuata kwa kuwa niliacha kuwatizama watu kwa jinsi ya mwili, bali nilianza kuwatambua kwa jinsi ya rohoni (2Wakorintho 5:16)

5. FURAHI SIKU ZOTE:
Siri ya ushindi katika matatizo yoyote, inatokana na furaha ya Kristo iliyo ndani ya mtu.
Neno la Mungu linasema, “Furahini katika Bwana siku zote, tena nasema, Furahini” (Wafilipi 4:4)

” Heri ninyi watakpowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia;kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu” (Mathayo 4:11, 12)

Huu ni ujumbe mzuri sana wa Bwana Yesu, kwa mtu wake aliyesongwa na maudhi pamoja na makwazo mbali mbali.
Inawezekana kuwa ndani ya nyumba yako una makwazo ya kila siku, kutokana na mume wako au mke wako ambaye hatembei katika nuru ya Kristo.
Na pia, inawezekana unapata maudhi sana juu ya tabia za watoto wako, ambao hawaenendi katika kweli ya neno la Mungu. Inawezekana unapata maudhi shuleni au kazini.

Hata kama umesongwa na makwazo na maudhi namna hiyo, Yesu Kristo , aliye bwana na Mwokozi wako, anakuambia. “FURAHI NA KUSHANGILIA“.
Furahi na kushangilia katika Bwana siku zote na katika yote. Hii ndiyo siri ya ushindi.
Kwa nini ufurahi na kushangilia?:
Kwa kuwa unafahamu kuwa mgomvi wako si mtu bali ni shetani. (Waefeso 2:1-3).

Kwa kuwa unafahamu kuwa anayekuudhi si mume wako, wala mke wako, wala watoto wako, bali ni shetani anayewatumia kutaka kukukasirisha wewe, ili umkosee Mungu wako.
Kwa kuwa unafahamu kuwa shetani ameshindwa; na wewe una mamlaka juu yake na maudhi yake yote (Luka 10:19)
Kwa hiyo ufanyeje?

Furahi na kushangilia moyoni mwako.
Kumbuka kuwa Kristo aliye ndani yako ni mkuu kuliko shetani na makwazo yake na maudhi yake (1Yohana 4:4).
Furahi na kushangilia unapoudhiwa, na mtolee Mungu shukrani kwa nyimbo za sifa.

Fanya hivyo na hasira haitapata nafasi moyoni mwako, wala uchungu wo wote.
Tumia tabia ya Kristo iliyo ndani yako ya kuwaombea wanaokuudhi, kama vile yeye alivyosema pale msalabani, “Baba uwasemehe kwa maana hawajui walitendalo“.

Baada ya kufurahi na kushangilia na kusifu, kitu gani kinafuata?
Upole wako ujulikane na watu wote” (Wafilipi 4:5)
Na upole ni tunda la Roho. Na kazi ya roho ya upole ni kutuliza maudhi. (Mhubiri 10:4)

Wakati wa maudhi ndiyo wakati mzuri wa kumdhihirisha Kristo aliye ndani yako katika upole wote na utulivu.
Usijisumbue na kuhangaika katika neno lo lote, bali katika kila jambo, kwa kusali na kuomba na kushukuru, haja yako na ijulikane na Mungu (Wafilipi 4:6).
Usiwe mwepesi kumwambia mtu maudhi ya nyumbani mwako, au ofisini mwako. Utajikuta umeingia katika kusengenya na hutafaulu kamwe kujifunza kusamehe.

Maudhi na makwazo yapeleke kwa Bwana. Yeye anatosha kukushindia.
Fanya hivyo, na amani ipitayo akili na fahamu zote na maudhi na makwazo itakuhifadhi na kukufariji moyo wako siku zote katika Bwana (Wafilipi 4:7)
Nilikuwa mahali fulani nikifundisha neno la Mungu, na kila siku niliombea wagonjwa. Basi, siku moja mama mmoja alisimama kushuhudia alivyopona.

Na haya ndiyo aliyosema:
Nina uhakika kuwa ugonjwa huu niliokuwa nao ulikuja kwa sababu ya dhambi nilizokuwa nazo. Mimi sikushikwa na dhambi zingine kama wengine wanavyoshikwa. Mimi nilishikwa na dhambi hii.
Mume wangu huwa hanipi fedha ya kununulia chumvi nyumbani. Basi nilichukia sana; na mimi nikipata fedha na kununua chumvi, naificha nje ya nyumba. Mimi na watoto tunakula chakula chenye chumvi. Mume wangu namtengea chakula kisichokuwa na chumvi.“

Na niliwambia watoto ye yote atakayesema hayo kwa baba yake atachapwa.Lakini nilipoanza kufanya hivyo nilianza kuugua mara kwa mara, na hapa kwenye mkutano huu nimekuja na mguu umevimba na kunisababisha nisitembee vizuri.

Baada ya kusikia neno la Mungu nilifahamu kuwa ugonjwa huu nimeupata kwa sababu ya kosa hilo la kumkasirikia mume wangu.
Nikamsamehe mume wangu. Nikatubu kwa Mungu. Na maombezi ya wagonjwa yalipofanywa nilijikuta nimeanguka chini. Nilipoamka nilikuta uvimbe mguuni umetoweka. Na sasa nimepona na natembea vizuri.
Nikirudi nyumbani nitamwambia mume wangu yote, na nitamwomba anisamehe”.

Hii ndiyo nguvu ya uponyaji ya neno la Mungu inayoshuka baada ya kusamehe. Roho zinapona, miili inapona na ndoa zinapona! Yule mama alisamehe kwanza ndipo akapokea uponyaji.
Na wewe sasa, samehe na kusahau upokee uponyaji wako au upokee majibu ya maombi yako.

Kumbuka kabla ya kusimama na kusali samehe kwanza. Hii ni kwa ajili yako mwenyewe, ili usamehewe na Mungu na upokee unaloomba siku zote.