“Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali YATAFAKARI MANENO YAKE MCHANA NA USIKU, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapofanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.” (Yoshua 1:8)

Mtu mmoja aliwahi kuniuliza swali hili: “Je kutafakari maana yake nini?” Kila mara ninapofundisha somo hili nakutana na swali la jinsi hii .

Naamini kuwa swali hili linawatatanisha wengi kwa sababu bado hawajatofautisha kati ya kusoma neno na kutafakari neno.

Kusoma neno ni tofauti na kutafakari neno. Kulitafakari neno ni zaidi ya kulisoma neno. Watu wengi huwa wanasoma neno zaidi kuliko kulitafakari.

Kutafakari maana yake nini?
Maana ya karibu sana ya neno kutafakari ni kuwaza. Ni kusoma neno huku unalicheua na kulitafuna rohoni mwako.

Kutafakari ni njia mojawapo kubwa ya kuweza kuilisha roho yako. Yesu Kristo alisema “Imeandikwa, mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.” (Mathayo 4:4)
Mkate ni chakula cha mwili wa nje ulio wa nyama na damu; neno la Mungu ni chakula cha mwili wa kiroho. Kinywa kinapokea chakula na meno yanatafuna.na kukivunjavunja huku kikilainishwa na mate, tayari kwa kumeza.

Kusoma neno ni kama kinywa, kazi yake ni kulipokea neno. Kutafakari ni kuvunjavunja hilo neno huku Roho wa Mungu akililainisha liwe tayari kumezwa na roho yako.

Kutafakari neno kunamletea mtu siri ya ajabu ya uhakika na ushindi ndani ya Kristo.

Sisi ni watenda kazi pamoja na neno la Mungu hapa ulimwenguni. Tunaliwakilisha Neno la Kristo mahali tulipo na ulimwenguni pote.

Na kwa sababu hiyo, Imeandikwa, “Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote.” (Wakolosai 3:16)

Huwezi ukawa na Neno la Kristo moyoni mwako bila ya kuitumia siri ya kutafakari. Kukariri neno la Kristo hakutoshi peke yake kukuletea uhakika na ushindi kiroho na kimwili kama vile kutafakari kunavyofanya ndani ya mtu.

Kutafakari ni kuwaza. Kulitafakari jina la Yesu Kristo ni kuliwaza jina hili.

Tatizo kubwa sana ambalo linawapata watu ni tatizo la mawazo. Na huu ni ugonjwa mkubwa sana ambao umewakwamisha wengi katika maisha yao ya kiroho.

Kutafakari na kuwaza ni jambo la rohoni, - ni jambo la rohoni! Si jambo la akili kama wengi wanavyodhani.

Mtu anapowaza, au kutafakari jambo huwa ni jambo linalofanyika rohoni mwake, ingawa utadhani linafanyika katika ubongo.

Je! Wewe unayesoma somo hili sasa hivi unawaza nini rohoni mwako, unatafakari nini? Mara nyingi utaona mtu anaposoma Neno mawazo yake mara nyingi yanakuwa mbali sana, kwa hiyo hakuna anachoelewa katika hayo anayosoma.

Pia, hata wakati watu wanasikiliza neno la Mungu, mara nyingi mawazo yao yanakuwa mbali sana na neno linalofundishwa. Hii inajidhihirisha hasa ukimwuuliza mtu huyo muda mchache baadaye, juu ya neno lililofundishwa maana hatakumbuka.

Unapoumwa huwa unawaza nini? Wengi wanautafakari ugonjwa, na wengine hata kukata tamaa anapoona hauponi haraka. Wengine wanapoumwa wanawaza na kutafakari kufa kuliko kuishi.

Unapokuwa una matatizo huwa unawaza nin? Unapokosa maelewano na mwenzako, nyumbani, kazini au mahali popote, huwa mawazo yako yanawaza nini?

Unapokuwa huna fedha au vitu fulani vya kimwili huwa unawaza au kutafakari nini?

Tunaweza kusema mengi lakini swali kubwa ni hili; “Kila wakati huwa unawaza nini na kutafakari nini?”

Je! unafahamu ya kuwa matendo yako na maneno yako , ni matokeo ya mawazo uliyonayo? Mtu husema anachokitafakari au kukiwaza, na pia hutenda anachokitafakari au kukiwaza moyoni mwake.

Ukitaka kumfahamu mtu alivyo rohoni mwake, sikiliza maneno anayosema na angalia matendo anayoyatenda.